Thursday, 27 April 2017

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee  na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa kuhusu Usawa wa Kijinsia lililoandaliwa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam(DUCE) leo Jijini Dar es Salaam. Waziri Ummy alimwakilisha Makamu wa Rais katika ufunguzi wa Kongamano hilo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiteta jambo na  Makamu Mkuu wa Chuo Kiku u cha Dar es Salaam(UDSM) Profesa Rwekaza Mukandala wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa kuhusu Usawa wa Kijinsia lililoandaliwa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam(DUCE) leo Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Kimataifa kuhusu Usawa wa Kijinsia lililoandaliwa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam(DUCE) wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu(hayupo pichani) alipomwakilisha Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wawasilisha mada katika Kongamano la Kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia mara baada ya ufunguzi wa kongamano hilo leo Jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo la siku mbili limeandaliwa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).


NA ANTHONY ISHENGOMA- WIZARA YA AFYA
Uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari umewanufaisha wanafunzi wa kike ambao walikuwa wanakosa fursa hiyo kwasababu baadhi ya wazazi walikuwa wanatoa kipaumbele kwa watoto wa kiume.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akifungua Kongomano la kwanza la Kimataifa la Kijinsia la Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) alipomwakilisha Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Jijini Dar es Saalam.

Waziri Ummy amewataka baadhi ya wananchi kutobeza uamuzi huo kwani unatoa fursa zaidi kwa mtoto wa kike kunufaika na elimu tofauti na awali ambapo baadhi ya familia kwasababu ya umasikini  zilitoa kipaumbele kwa mtoto wa kiume.

Aliongeza kuwa kuna madai yakuongezeka kwa idadi ya wanafunzi akisema ongezeko hilo limetokana na kuwepo kwa fursa ya elimu bure ambayo imewezesha watoto walikuwa wanabaki nyum bani kutokana na umasikini kufaidika na uamzi wa serikali ya wamu ya tano kutoa elimu bure.

Amekitaka Chuo Kikuu kishiriki DUCE kufanya utafiti ili kujua watoto hawa waliosababisha ongezeko hilo wanatoka familia za aina gani ili kuiwezesha serikali kuweka mipango endelevu ya utoaji elimu hususani kwa watoto wanaotoka kaya masikini.

Aidha Waziri kuna baadhi ya watu bado wanadhani wazo la kuwarejesha watoto wakike shuleni baada ya kujifungua ni kuhamasisha uhuni akisema lengo la serikali ni kumsomesha mtoto wa kike bila kujali mazingira yanayomzunguka kwasababu watoto wakike kutoka familia tajiri wanapopata ujauzito uhamishiwa na shule binafsi na kuendelea na masomo tofauti na mwanafunzi wakike kutoka kaya masikini.

Amekipongeza chuo kikuu cha Dar es Salaam kwa kudahili wanafunzi wakike kwa asilimia 38 akiwataka kufikia 50 kwa 50 ifikapo 2025 na kuhimiza watoto wakike kushiriki katika masomo ya sayansi kwani takwimu zinaonesha udahili katika masomo ya sayansi katika elimu ya juu bado yako chini ukilinganisha na wanaume.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Pofesa Rwekaza Mukandala wakati akitoa hotuba yake kwa mgeni rasmi amesema kuwa tatizo la unyanyasaji na ukosefu wa fursa sawa kijinsia ni tatizo la kihistoria duniani kote na kusema kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitaendelea kufanya tafiti na kutoa elimu ya masuala ya kijinsia ili kukabiliana na tatizo hilo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu. 

Naye Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) Profesa William Anangisye amesema tangu kuanzishwa kwa DUCE zimekuwepo juhudi mbalimbali za kuwatafuta wanazuoni kutoka nchi mbalimbali kufika chuoni hapo ili waweze kufundisha na kuzungumzia masuala mbalimbali ya elimu ya kijinsia na usawa katika elimu ya juu.

Amewaambia washiriki kongomano hilo lasiku mbili kuwa kuna washiriki kutoka zaidi ya nchi ishirini na tano na linalenga kutoa matokeo ya tafiti mbalimbali za elimu ya kijinsia kwa jamii na kutoa fursa muhimu miongoni mwa wanazuoni kujadili matokeo ya tafiti hizo. 


Thursday, 9 March 2017

maaadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ni hatua muhimu kwa wanawake kujipambanua na kufanya tathmini jinsi wanavyoshiriki katika ujenzi wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Serikali imeweka mikakati na mipango mbalimbali yenye lengo la kumkomboa na kumuinua mwanamke kiuchumi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, mama Sihaba Nkinga hivi karibuni alipokuwa akizungumzia mipango na mikakati mbalimbali iliyofanywa na Serikali katika kumkomboa na kumuinua mwanamke kiuchumi.

Pamoja na kuwa wanawake wengi wameamka na wanajishughulisha katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, Serikali pia inahakikisha inawawezesha ili waweze kufikia malengo yao katika masuala ya kujiinua kiuchumi na kuondokana na dhana ya utegemezi.

“Serikali ina mipango mbalimbali katika kuhakikisha kuwa wanawake wamewezeshwa kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha benki ya Wanawake ambayo moja ya majukumu yake ni kuhakikisha wanawake wanapata mikopo kwa kuzingatia viwango wanavyoweza kulipa” alisema mama Nkinga.

Aliitaja mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuwa na mfuko wa maendeleo ya wanawake ambapo wanawake wanapewa mikopo yenye riba nafuu ambayo wanamudu kuilipa.

Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kuwasaidia wanawake katika masuala ambayo yamekuwa yakiwasumbua kwa muda mfefu kama vile umiliki wa ardhi. Kupitia elimu hii kwa sasa wanawake wanaruhusiwa kumiliki ardhi kisheria na kuondoa utata kuhusu suala hili.

Pamoja na mikakati hiyo, Serikali imeenelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kuwa vikwazo mbali mbali vya mitaji na mikopo vinaondolewa ili kuhakikisha kuwa wanawake wengi wanapata fursa ya kukopa na kulipa kwa muda hivyo kuwa huru kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.

“Idadi kubwa ya wakina mama wapo kwenye ujasiriamali na viwanda vidogo vidogo hivyo Serikali imekuwa ikitoa elimu kwao na kuwahimiza kukopa kwenye vyombo na taasisi za fedha kwa sababu huko wanakopa kulingana na uwezo wao na hii itawasaidia kufanikisha shughuli zao za ujasiriamali“ aliongeza mama Sihaba .

Aliwaasa wanawake kuachana na sekta isiyo rasmi na badala yake wajikite katika sekta rasmi maana huko kuna uzalishaji mkubwa ambao utawapatia soko la nje na aliwataka kuboresha bidhaa zao ili wawe tayari katika ushindani mkubwa zaidi wakati nchi yetu ikielekea katika uchumi wa viwanda.

Akizungumzia fursa na mlingano wa ajira kati ya wanawake na wanaume alisema kuwa upande wa ajira wote wanawake na wanaume wana nafasi sawa na kinachozingatiwa ni vigezo na sifa za waombaji wa ajira.

Katibu Mkuu huyo aliendelea kusema kwa sasa hakuna kazi za wanaume peke kwani upo uhalisia juu ya ushiriki wa wanawake wengi katika kazi za uhandisi, ukandarasi na udaktari.

Alitoa wito kwa wanawake, jamii na watanzania kwa ujumla kuitumia siku hii kutoa hamasa kwa wanawake na kuangalia nafasi yao katika jamii kipindi hiki ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati na viwanda.

Ili kufikia azma ya uchumi wa viwanda, ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha anadumisha Umoja wa nchi yetu na Utanzania wetu kwa kuwashirikisha wanawake, kwa kutoa elimu na kuwapa nafasi ili watoe mchango wao ipasavyo katika kuinua uchumi wa nchi.

Aidha, mama Nkinga alihimiza jamii kusimamia watoto wa kike na kuhakikisha wanapewa haki inayostahili ili nao wafike mahali waweze kutoa mchango wao kwa taifa.

Siku ya wanawake duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 8, Machi kwa shughuli mbalimbali kama vile maandamano na hotuba, pia wanawake hutumia nafasi hiyo kutathmini mafanikio ya shughuli zao za maendeleo, changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo. Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Tanzania ya viwanda, wanawake ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi.”
Waziri wa afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu akikata utepe kuzindua kituo na kiwanda cha kuongeza thamani mazao ya nafaka cha Ititi kinachomilikiwa na vikundi vya akina mama VICOBA wa wilaya ya Singida, kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkazi wa shirika la UN women Tanzania  Maria Karadenizli.
.Waziri wa afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu akionyesha ndoo ambayo ni kifungashio cha mafuta ya alizeti yanayozalishwa katika kiwanda cha mount Meru millers Mkoani Singida
Waziri wa afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi wakikagua kiwanda cha mafuta  cha Mount Meru Millers kilichopo mjini Singida, kiwanda hicho huzalisha mafuta ya alizeti ambayo ni mazuri kwa afya
Waziri wa afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi wakikagua hatua za uongezaji wa thamani wa mazao ya nafaka kama mahindi, mtama na uwele katika kiwanda kinachomilikiwa na kikundi cha akina mama VICOBA wa Wilaya ya Singida


Tuesday, 7 March 2017









TAARIFA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO MHE. UMMY ALLY MWALIMU (MB) KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI YA MACHI 8, MWAKA 2017









Nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa itaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 8 Machi, 2017 na kwa mwaka huu itafanyika katika ngazi ya mkoa kwa kuzingatia amzingira ya mkoa husika.

Aidha Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka 2017 ni TANZANIA YA VIWANDA: WANAWAKE NI MSINGI WA MABADILIKO YA KIUCHUMI”. Kaulimbiu hii imetoholewa kutokana na Kaulimbiu ya Kipaumbele ya Umoja wa Mataifa mwaka huu katika Mkutano wa 61 wa Hali ya Wanawake Duniani (CSW) inayosema Women Economic Empowerment in the Changing World of Work” ambayo tafsiri yake kwa lugha ya kiswahili ni “Uwezeshaji Wanawake: Kiuchumi Katika Dunia ya Mabadiliko ya Kazi”.

Kaulimbiu hii ya “Tanzania ya Viwanda: Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko ya Kiuchumi” inalenga kuhamasisha jamii, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi, Taasisi za Serikali, Vyama vya Siasa, Wabia wa Maendeleo, mtu mmoja mmoja na wadau wengine hapa nchini Tanzania kuongeza wigo wa fursa za kiuchumi kwa wanawake ili kuwawezesha kushiriki na kunufaika na hatua za maendeleo katika kipindi hiki ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati na wa viwanda.

Chimbuko la kuanzishwa kwa Siku ya Wanawake lilianza mwanzoni mwa miaka ya 1900 kufuatia maandamano ya wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini Marekani kupinga mazingira duni ya kazi. Waandamaji hao, walilalamikia ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira ikiwemo wanawake kulipwa mshahara mdogo kwa kazi sawa ukilinganisha na wanaume.

Kwa kuzingatia hali hiyo, Umoja wa Mataifa baada kuanzishwa mwaka 1945 uliridhia kuwa tarehe 8 Machi kila mwaka iwe ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani. Uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kuanzisha Siku ya Wanawake Duniani ulitokana na ukweli kwamba masuala ya haki, maendeleo na usawa wa wanawake yalihitaji msukumo maalumu na wa kipekee.

Lengo kuu la kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kutoa fursa kwa jamii kupima utekelezaji wa maazimio, matamko, mikataba na itifaki mbalimbali za Kimataifa, kikanda  na kitaifa zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia na uwezeshaji wanawake. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa haki za wanawake kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa zinapatikana na zinalindwa.

Kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua na kuthamini uwezo na mchango mkubwa wa wanawake katika kuleta maendeleo pamoja na kuelezea jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo yao, familia zao, jamii na Taifa kwa ujumla.

Aidha wanawake ni kundi kubwa na muhimu katika jamii (asilimia 51 ya Watanzania Wote) na kwamba hakuna maendeleo yeyote yanayoweza kufikiwa ikiwa kundi hili litaachwa nyuma.

Kwa mantiki hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha wanawake wanashiriki na kunufaika na uchumi hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu imejipanga kuelekea katika uchumi wa viwanda na kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Taarifa ya Jukwaa la Uchumi Duniani kuhusu ‘Pengo la Jinsia ya Mwaka 2016’ inaonesha kuwa kutokana na jitihada zilizofanyika nchi yetu inashika nafasi ya 53 kati ya nchi 144 zinazofanya vizuri katika masuala ya jinsia Duniani. 

Katika jitihada za  kuwawezesha wanawake kiuchumi Serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ambao unatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wajasiriamali wadogo kuanzisha na kuendeleza biashara, viwanda vidogo, kilimo pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi.

Aidha kupitia Mfuko huo, Halmashauri zimehamasishwa kuchangia asilimia tano ya mapato yao ya ndani ambapo katika kipindi cha Julai hadi Disemba, 2016 kiasi cha shs. 4,102,808,513 kilitolewa kwa vikundi vya wanawake na vijana katika Halmashauri 101 kupitia utaratibu huu.

Benki ya Wanawake Tanzania pia ilitoa mikopo yenye thamani ya Shs 9,323,240,000/-  kwa wajasiriamali 6,267 kati ya hao wanawake walikuwa 4,596. Hivyo, kiasi cha mikopo iliyotolewa imeongezeka kutoka Tshs. 112,473,600,000/- mwaka 2015 hadi kufikia Shs  121,796,840,000/-  mwaka 2016.

Aidha, idadi ya wajasiriamali waliopata na kunufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya Wanawake Tanzania iliongezeka kutoka wajasiriamali 79,983 mwaka 2015 hadi kufikia wajasiriamali 86,250 mwaka 2016 ambapo asilimia 73 ya wanufaika wa mikopo hiyo ni wanawake.

Kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika fursa mbalimbali za kiuchumi, Serikali imeratibu na kuzindua majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi. Majukwaa haya yatatumika kama sehemu muhimu kwa wanawake wajasiriamali kukutana na kujadili fursa za kiuchumi pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili na namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo.

Aidha, sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2002, (ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2007) imetoa fursa sawa za ajira kati ya wanawake na wanaume. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, pale inapotokea mwanaume na mwanamke wanapata alama sawa wakati wa usaili, mwanamke anapewa kipaumbele kupata nafasi hiyo.

Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini (2004) imetoa fursa sawa kati ya wanawake na wanaume kuhusu haki zao za ajira, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa likizo ya uzazi kwa wanawake na wanaume.

Kwa kutambua elimu na mafunzo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha wanawake na wanaume wanashiriki na kunufaika ipasavyo na uchumi wa viwanda, Serikali imeendelea kuhakikisha kila mtanzania anapata elimu kama haki ya msingi.

Katika kuhakikisha kuwa mtoto wa kike na wa kiume wanapata haki ya elimu, Serikali inatekeleza sera ya Elimu bila malipo ambayo inatoa fursa ya Elimu ya Msingi na ya Sekondari na kuwahakikishia watoto elimu hiyo bila kujali tofauti za kiuchumi.

Sera hii imeleta mafanikio makubwa katika eneo hili ambapo takwimu zinaonesha kuwapo ongezeko la udahili kwa watoto wa kike na kiume

Pamoja na masuala yote yaliyotajwa hapo juu Kumekuwepo na ongezeko la ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi. Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1995 na ya mwaka 2005 yalifanywa na kuongeza idadi ya viti maalum kwa wanawake vilivyoongezwa hadi kufikia asilimia 30. 

Katika kuhakikisha kuwa wanawake wanajengewa uwezo wa kisheria na kupata haki zao, sheria kadhaa zimetungwa na nyingine kufanyiwa marekebisho ikiwemo Sheria ya Makosa ya Kujamiiana yaani (SOSPA) ya  mwaka 1998, ambayo imefanyiwa marekebisho  na kuhuishwa kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu.

Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo imetoa fursa sawa katika ajira na likizo ya Uzazi pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009; Sheria ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999, ambapo sheria hii inampa mwanamke haki ya kumiliki na kurithi ardhí sawa wanaume.

Pia, katika mwaka 2016/17 Bunge la Jamhuria ya Muungano limepitisha Sheria ya Msaada wa Sheria ya mwaka 2016 ambayo itasawadia wanawake hasa wenye kipato cha chini kupata haki zao za msingi.

Serikali inatambua kuwa ukatili dhidi ya wanawake bado ni tatizo kubwa ambalo linaathiri ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na kijamii. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 – 2021/22) ambao ulizinduliwa tarehe 13 Disemba, 2016.

IMETOLEWA NA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO