TAARIFA
YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO MHE. UMMY ALLY
MWALIMU (MB) KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE
DUNIANI YA MACHI 8, MWAKA 2017
Nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine
wanachama wa Umoja wa Mataifa itaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambayo kilele
chake kitakuwa tarehe 8 Machi, 2017 na kwa mwaka huu itafanyika katika ngazi ya
mkoa kwa kuzingatia amzingira ya mkoa husika.
Aidha Kaulimbiu ya maadhimisho ya
mwaka 2017 ni “TANZANIA YA
VIWANDA: WANAWAKE NI MSINGI WA MABADILIKO YA KIUCHUMI”. Kaulimbiu
hii imetoholewa kutokana na Kaulimbiu ya
Kipaumbele ya Umoja wa Mataifa mwaka huu katika Mkutano wa 61 wa Hali ya
Wanawake Duniani (CSW) inayosema “Women Economic Empowerment in the Changing
World of Work” ambayo tafsiri yake kwa lugha ya kiswahili ni “Uwezeshaji Wanawake: Kiuchumi Katika Dunia
ya Mabadiliko ya Kazi”.
Kaulimbiu hii ya “Tanzania ya Viwanda: Wanawake ni Msingi wa
Mabadiliko ya Kiuchumi” inalenga kuhamasisha jamii, Asasi za Kiraia, Sekta
Binafsi, Taasisi za Serikali, Vyama vya Siasa, Wabia wa Maendeleo, mtu mmoja
mmoja na wadau wengine hapa nchini Tanzania kuongeza wigo wa fursa za kiuchumi
kwa wanawake ili kuwawezesha kushiriki na kunufaika na hatua za maendeleo
katika kipindi hiki ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati na wa
viwanda.
Chimbuko la kuanzishwa kwa Siku ya Wanawake lilianza mwanzoni mwa
miaka ya 1900 kufuatia maandamano ya wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda
nchini Marekani kupinga mazingira duni ya kazi. Waandamaji hao, walilalamikia
ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira
ikiwemo wanawake kulipwa mshahara mdogo kwa kazi sawa ukilinganisha na wanaume.
Kwa kuzingatia hali hiyo, Umoja wa Mataifa
baada kuanzishwa mwaka 1945 uliridhia kuwa tarehe 8 Machi kila mwaka iwe ni
Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani. Uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kuanzisha
Siku ya Wanawake Duniani ulitokana na ukweli kwamba masuala ya haki, maendeleo
na usawa wa wanawake yalihitaji msukumo maalumu na wa kipekee.
Lengo kuu la kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni
kutoa fursa kwa jamii kupima utekelezaji wa maazimio, matamko, mikataba na
itifaki mbalimbali za Kimataifa, kikanda
na kitaifa zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia na uwezeshaji
wanawake. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa haki za wanawake kiuchumi, kijamii,
kiutamaduni na kisiasa zinapatikana na zinalindwa.
Kuadhimisha
Siku ya Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua na
kuthamini uwezo na mchango mkubwa wa wanawake katika kuleta maendeleo pamoja na
kuelezea jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau mbalimbali
katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu
katika kujiletea maendeleo yao, familia zao, jamii na Taifa kwa ujumla.
Aidha wanawake ni
kundi kubwa na muhimu katika jamii (asilimia 51 ya Watanzania Wote) na kwamba
hakuna maendeleo yeyote yanayoweza kufikiwa ikiwa kundi hili litaachwa nyuma.
Kwa mantiki hiyo, Serikali
kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha
wanawake wanashiriki na kunufaika na uchumi hasa katika kipindi hiki ambacho
nchi yetu imejipanga kuelekea katika uchumi wa viwanda na kuwa nchi ya uchumi
wa kati.
Taarifa ya Jukwaa
la Uchumi Duniani kuhusu ‘Pengo la Jinsia ya Mwaka 2016’ inaonesha kuwa
kutokana na jitihada zilizofanyika nchi yetu inashika nafasi ya 53 kati ya nchi
144 zinazofanya vizuri katika masuala ya jinsia Duniani.
Katika jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi Serikali
imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ambao unatoa mikopo yenye masharti
nafuu kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wajasiriamali wadogo kuanzisha na
kuendeleza biashara, viwanda vidogo, kilimo pamoja na shughuli nyingine za
kiuchumi.
Aidha kupitia Mfuko huo, Halmashauri
zimehamasishwa kuchangia asilimia tano ya mapato yao ya ndani ambapo katika
kipindi cha Julai hadi Disemba, 2016 kiasi cha shs. 4,102,808,513 kilitolewa kwa vikundi vya wanawake na vijana
katika Halmashauri 101 kupitia utaratibu huu.
Benki ya Wanawake Tanzania pia
ilitoa mikopo yenye thamani ya Shs
9,323,240,000/- kwa wajasiriamali
6,267 kati ya hao wanawake walikuwa 4,596. Hivyo, kiasi cha mikopo iliyotolewa
imeongezeka kutoka Tshs.
112,473,600,000/- mwaka 2015 hadi kufikia Shs 121,796,840,000/- mwaka 2016.
Aidha, idadi ya wajasiriamali
waliopata na kunufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya Wanawake Tanzania
iliongezeka kutoka wajasiriamali 79,983 mwaka 2015 hadi kufikia wajasiriamali
86,250 mwaka 2016 ambapo asilimia 73 ya wanufaika wa mikopo hiyo ni wanawake.
Kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa
wanawake katika fursa mbalimbali za kiuchumi, Serikali imeratibu na kuzindua
majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi. Majukwaa haya yatatumika kama sehemu
muhimu kwa wanawake wajasiriamali kukutana na kujadili fursa za kiuchumi pamoja
na changamoto mbalimbali zinazowakabili na namna bora ya kukabiliana na
changamoto hizo.
Aidha, sheria ya Utumishi wa Umma ya
Mwaka 2002, (ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2007) imetoa fursa sawa za ajira
kati ya wanawake na wanaume. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, pale inapotokea
mwanaume na mwanamke wanapata alama sawa wakati wa usaili, mwanamke anapewa
kipaumbele kupata nafasi hiyo.
Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini
(2004) imetoa fursa sawa kati ya wanawake na wanaume kuhusu haki zao za ajira,
ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa likizo ya uzazi kwa wanawake na wanaume.
Kwa
kutambua elimu na mafunzo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha wanawake na
wanaume wanashiriki na kunufaika ipasavyo na uchumi wa viwanda, Serikali
imeendelea kuhakikisha kila mtanzania anapata elimu kama haki ya msingi.
Katika kuhakikisha kuwa mtoto wa
kike na wa kiume wanapata haki ya elimu, Serikali inatekeleza sera ya Elimu
bila malipo ambayo inatoa fursa ya Elimu ya Msingi na ya Sekondari na
kuwahakikishia watoto elimu hiyo bila kujali tofauti za kiuchumi.
Sera hii imeleta mafanikio makubwa
katika eneo hili ambapo takwimu zinaonesha kuwapo ongezeko la udahili kwa
watoto wa kike na kiume
Pamoja na
masuala yote yaliyotajwa hapo juu Kumekuwepo na ongezeko la ushiriki wa wanawake katika
ngazi mbalimbali za maamuzi. Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1995 na ya mwaka 2005 yalifanywa na kuongeza idadi ya viti
maalum kwa wanawake vilivyoongezwa hadi kufikia asilimia 30.
Katika kuhakikisha kuwa wanawake wanajengewa uwezo wa
kisheria na kupata haki zao, sheria kadhaa zimetungwa na nyingine kufanyiwa
marekebisho ikiwemo Sheria ya Makosa ya
Kujamiiana yaani (SOSPA) ya mwaka 1998,
ambayo imefanyiwa marekebisho na
kuhuishwa kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu.
Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini
Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo imetoa fursa sawa katika ajira na likizo ya Uzazi
pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009; Sheria ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya
Vijiji ya mwaka 1999, ambapo sheria hii inampa mwanamke haki ya kumiliki na
kurithi ardhí sawa wanaume.
Pia, katika mwaka 2016/17 Bunge la
Jamhuria ya Muungano limepitisha Sheria ya Msaada wa Sheria ya mwaka 2016
ambayo itasawadia wanawake hasa wenye kipato cha chini kupata haki zao za msingi.
Serikali
inatambua kuwa ukatili dhidi ya wanawake bado ni tatizo kubwa ambalo linaathiri
ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na kijamii. Katika kukabiliana
na tatizo hilo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa Mpango
Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 –
2021/22) ambao ulizinduliwa tarehe 13 Disemba, 2016.
IMETOLEWA
NA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO
0 comments:
Post a Comment