maaadhimisho
ya Siku ya Wanawake Duniani, ni hatua muhimu kwa wanawake kujipambanua
na kufanya tathmini jinsi wanavyoshiriki katika ujenzi wa taifa
kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Serikali imeweka mikakati na mipango mbalimbali yenye lengo la kumkomboa na kumuinua mwanamke kiuchumi.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto,
mama Sihaba Nkinga hivi karibuni alipokuwa akizungumzia mipango na
mikakati mbalimbali iliyofanywa na Serikali katika kumkomboa na kumuinua
mwanamke kiuchumi.
Pamoja
na kuwa wanawake wengi wameamka na wanajishughulisha katika masuala
mbalimbali ya kiuchumi, Serikali pia inahakikisha inawawezesha ili
waweze kufikia malengo yao katika masuala ya kujiinua kiuchumi na
kuondokana na dhana ya utegemezi.
“Serikali
ina mipango mbalimbali katika kuhakikisha kuwa wanawake wamewezeshwa
kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha benki ya Wanawake ambayo moja ya
majukumu yake ni kuhakikisha wanawake wanapata mikopo kwa kuzingatia
viwango wanavyoweza kulipa” alisema mama Nkinga.
Aliitaja
mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuwa na mfuko wa maendeleo ya
wanawake ambapo wanawake wanapewa mikopo yenye riba nafuu ambayo
wanamudu kuilipa.
Aidha,
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kuwasaidia
wanawake katika masuala ambayo yamekuwa yakiwasumbua kwa muda mfefu kama
vile umiliki wa ardhi. Kupitia elimu hii kwa sasa wanawake wanaruhusiwa
kumiliki ardhi kisheria na kuondoa utata kuhusu suala hili.
Pamoja
na mikakati hiyo, Serikali imeenelea kushirikiana na wadau kuhakikisha
kuwa vikwazo mbali mbali vya mitaji na mikopo vinaondolewa ili
kuhakikisha kuwa wanawake wengi wanapata fursa ya kukopa na kulipa kwa
muda hivyo kuwa huru kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.
“Idadi
kubwa ya wakina mama wapo kwenye ujasiriamali na viwanda vidogo vidogo
hivyo Serikali imekuwa ikitoa elimu kwao na kuwahimiza kukopa kwenye
vyombo na taasisi za fedha kwa sababu huko wanakopa kulingana na uwezo
wao na hii itawasaidia kufanikisha shughuli zao za ujasiriamali“
aliongeza mama Sihaba .
Aliwaasa
wanawake kuachana na sekta isiyo rasmi na badala yake wajikite katika
sekta rasmi maana huko kuna uzalishaji mkubwa ambao utawapatia soko la
nje na aliwataka kuboresha bidhaa zao ili wawe tayari katika ushindani
mkubwa zaidi wakati nchi yetu ikielekea katika uchumi wa viwanda.
Akizungumzia
fursa na mlingano wa ajira kati ya wanawake na wanaume alisema kuwa
upande wa ajira wote wanawake na wanaume wana nafasi sawa na
kinachozingatiwa ni vigezo na sifa za waombaji wa ajira.
Katibu
Mkuu huyo aliendelea kusema kwa sasa hakuna kazi za wanaume peke kwani
upo uhalisia juu ya ushiriki wa wanawake wengi katika kazi za uhandisi,
ukandarasi na udaktari.
Alitoa
wito kwa wanawake, jamii na watanzania kwa ujumla kuitumia siku hii
kutoa hamasa kwa wanawake na kuangalia nafasi yao katika jamii kipindi
hiki ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati na viwanda.
Ili
kufikia azma ya uchumi wa viwanda, ni jukumu la kila Mtanzania
kuhakikisha anadumisha Umoja wa nchi yetu na Utanzania wetu kwa
kuwashirikisha wanawake, kwa kutoa elimu na kuwapa nafasi ili watoe
mchango wao ipasavyo katika kuinua uchumi wa nchi.
Aidha,
mama Nkinga alihimiza jamii kusimamia watoto wa kike na kuhakikisha
wanapewa haki inayostahili ili nao wafike mahali waweze kutoa mchango
wao kwa taifa.
Siku
ya wanawake duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 8, Machi kwa
shughuli mbalimbali kama vile maandamano na hotuba, pia wanawake hutumia
nafasi hiyo kutathmini mafanikio ya shughuli zao za maendeleo,
changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo.
Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Tanzania ya viwanda, wanawake ni msingi
wa mabadiliko ya kiuchumi.”
0 comments:
Post a Comment