WIZARA YA AFYA MAENDELEO
YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAARIFA
KWA UMMA
MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI:8
MACHI, 2016
Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia,Wazee na watoto inawataarifu wananchi wote kuwa tarehe 8 Machi ya kila
mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa
kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake, hutoa fursa
kwa Serikali, wananchi, wadau, na wanawake wenyewe kupima utekelezaji wa
maazimio, matamko na mikataba ya Kimataifa, Kikanda na Kitaifa inayohusu
masuala ya maendeleo ya wanawake na usawa wa jinsia.
Siku ya wanawake Duniani
husisitiza kujenga mshikamano wa wanawake wote duniani, kuhamasisha jamii
kutafakari kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake ya kila mwaka;
kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na asasi
mbalimbali yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kuwaendeleza
wanawake; na kuhamasisha jamii kuhusu utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali
ya Serikali yenye lengo la kudumisha Amani, Usawa na Maendeleo.
Kaulimbiu ya
kitaifa ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2016 inasema “50 – 50 Ifikapo 2030; Tuongeze Jitihada”. Kaulimbiu hii inasisitiza kuwa na mikakati
thabiti yenye mwelekeo wa kufikia Agenda 2030 ya malengo inayohimiza kufikia asilimia
50 kwa 50 ya ushiriki wa wanawake na wasichana katika nyanja zote za maendeleo.
Kuanzia mwaka 2005 Serikali
ilipitisha uamuzi kuwa, maadhimisho haya yafanyike Kitaifa kila baada ya miaka mitano kutoa muda wa utekelezaji wa maazimio na kupima mafanikio
yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitano. Mwaka 2015 Maadhimisho
yalifanyika Kitaifa mkoani wa Morogoro. Kwa mwaka 2016, mikoa
yote itaadhimisha siku hii katika maeneo yao kwa kuzingatia hali na mazingira ya mikoa husika. Kwa mfano mkoa wa Dar
es salaam, utaadhimisha siku hii katika Manispaa ya Kinondoni. Wizara inatoa wito kwa mikoa yote kuhamasisha wananchi
na wadau wote kushiriki maadhimisho ya siku hii adhimu na kuzingatia ujumbe wa kauli
mbiu ya mwaka 2016.
Rai yangu kwa wadau wote ni kuwa, tuunge mkono jitihada za Serikali katika kutoa haki na
ushiriki sawa katika fursa za uongozi wa kisiasa na kiuchumi; na kupima
mafanikio yaliyofikiwa na kuweka mipango yenye matokeo makubwa, na kubainisha
shuhuda za wanawake waliotoa mchango uliotukuka katika kuwezesha maendeleo ya
wanawake wenywe na taifa kwa ujumla.
Nashauri wanahabari wote kuelimisha
jamii kuhusu kaulimbiu ya Siku ya Wanawake kwa mwaka 2016 ili kila mwananchi
aweze kutambua jukumu alionalo katika kufikia lengo la ushiriki sawa wa
wanawake na wasichana katika uchumi; afya, elimu, ajira, sheria na siasa ifikapo mwaka 2030.
Nawatakia
mafanikio mema katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu.
Sihaba Nkinga
KATIBU
MKUU
3/3/2016
0 comments:
Post a Comment