JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
(TAARIFA KWA UMMA)
WIZARA YALAANI MAUAJI YA MTOTO MARIAM DEOGRATIUS (4) ALIYEBAKWA NA KUUAWA ENEO LA MAKOKO, MUSOMA MKOANI MARA
Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inalaani vikali tukio la kubakwa na kuuawa kikatili
kwa mtoto Mariam Deoratius, umri miaka 4, ambaye alifanyiwa ukatili huo na watu
wasiojulikana, eneo la Makoko, Manispaa ya Musoma, mkoani Mara, mapema wiki hii.
Wizara imesikitishwa na mazingira ya
mauaji ya mtoto huyo mdogo asiyekuwa na hatia, ambaye aliokotwa kwenye banda
linalojengwa akiwa ameharibiwa sehemu zake za siri, kutokwa na damu nyingi na akiwa
amefariki dunia. Mauaji haya ni ukiukwaji mkubwa wa haki ya kuishi ya mtoto
ambayo ndiyo ni haki yake ya msingi. Haki hii inapovunjwa inarudisha nyuma
jitihada za Taifa letu kufanya jamii zetu kuwa mahali salama kwa watoto kuishi.
Wizara inaamini kuwa, Mamlaka zinazohusika na ulinzi wa watoto dhidi ya ukatili
katika Mkoa wa Mara hususan Manispaa ya Musoma, kuhakikisha mtuhumiwa
anafikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili haki iweze kutendeka, na kuwa
fundisho kwa wanaoendeleza ukatili wa watoto. Kwa tukio hili, jamii inahimizwa
kubadilika na kuhakikisha kuwa ulinzi wa watoto ni jukumu la wazazi, walezi na
watu wote katika jamii.
Wizara inatoa pole kwa wazazi, ndugu, marafiki na
familia ya mtoto Mariam aliyeuawa katika umri mdogo na tunawaomba kuwa wavumilivu
katika kipindi hiki kigumu.
Sihaba Nkinga
KATIBU
MKUU
0 comments:
Post a Comment