WIZARA ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imekabidhiwa
rasmi Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vipatavyo 55 kutoka Wizara ya Maendeleo,
Jinsia , Wazee na Watoto ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais Magufuli alilotoa
Aprili mwaka huu wakati akikabidhi hati idhini kwa Wizara hiyo ili kuendeleza
vyuo hivyo nchini.
Akiongea na waandishi wa habari wakati wa
makabidhiano ya nyaraka za makubaliano Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo,
Jinsia , Wazee na WatotoBi. Sihaba Nkinga amesema kuwa kukabdhiwa kwa vyuo
hivyo kwenye Wizara ya Elimu ni utekelezaji wa Agizo la Mhe. Rais Magufuli la
kuhamishia lililotolewa Aprili mwaka huu.
“Tumekabidhi rasmi vyuo vya maendeleo ya wananchi
mikononi mwa wizara ya Elimu kama alivyotuagiza Mh. Rais Aprili mwaka huu ili
visimamiwe kwa utaratibu mzuri pamoja na maendeleo yake kwa ajili ya wananchi
na taifa kwa ujumla” alisema Bi. Nkinga.
Aidha Bi. Nkinga amesema kuwa vyuo hivyo
vitaendelea na shughuli zake za kutoa elimu kwa wananchi kama ilivyokua zamani
ikiwa chini ya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kama ilivyoonyeshwa kwenye
hati idhini iliyotolewa na Mh. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu,Sayansi na Teknolojia Bi. Maimuna Tarish amesema kuwa Vyuo hivyo
vinatakiwa kuwa na ufundi stadi ambao upo kwenye viwango vya Wizara hiyo ili
kufikia uchumi wa kati hususani kwenye viwanda.
“Vyuo sasa vinatakiwa kutoa mafundi na wahandisi
wenye ufundi stadi ambao upo kwenye kiwango cha wizara ya Elimu ili kukidhi
teknolojia na kukuza uchumi wan chi kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda”
alisema Bi.Tarish.
Naye Mkuu wa Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Arnautoglu
Bi. Nsembia Mbwambo amesema kuwa wanaamini Wizara ya
Elimu itawapa muongozo mzuri zaidi kuongeza ufundi stadi kwa wanafunzi wa vyuo
hivyo.
Makabidhiano hayo yaliyofanywa na Wizara hizo
mbili ni makubaliano ya utekelezaji wa agizo la Mh. Rais lililotolewa Aprili
mwaka huu kuwa vyuo vyote vya maendeleo ya wananchi viratibiwe na Wizara ya
Elimu, Sayansi na teknolojia.
0 comments:
Post a Comment