TAMKO
LA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO MHE. UMMY
MWALIMU (MB.) KUHUSU WATOTO WALIOMALIZA ELIMU YA MSINGI LILILOTOLEWA
Ndugu Wanahabari,
Nitumie fursa hii kupitia kwenu kuongea na watoto wa
Tanzania, wazazi / walezi na jamii kwa ujumla katika kipindi hiki muhimu ambacho
watoto wetu wamemaliza Elimu ya Msingi. Kwa
niaba yangu na kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania napenda
kuchukua nafasi hii kuwapongeza watoto wote waliomaliza mtihani wa Taifa wa
kuhitimu Elimu ya Msingi mwaka huu, Hongereni
sana!. Ni jambo la ufahari kwetu sisi wote kama wazazi/ walezi na Taifa kwa
ujumla kwani hii ni fursa adhimu kwa ustawi na maendeleo ya mtoto na ni moja ya
njia ya kutimizwa kwa haki ya msingi ya mtoto ya kuendelezwa ambayo inamjengea
mtoto msingi imara wa maisha yake ya baadae. Pongezi zangu nyingi kwa watoto
wote wa kike na wa kiume walioweza kufikia hatua hii muhimu kwa maendeleo na
ustawi wao.
Ndugu Wanahabari,
Takwimu zinaonyesha kuwa, wanafunzi 795,761 (wavulana 372,883
sawa na asilimia 46.86 na wasichana 422,878 sawa na asilimia 53.14) wamesajiliwa
kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu. Hivyo ningependa kutumia fursa hii
kuwaasa watoto waliomaliza darasa la saba kutojihusisha na tabia au vitendo
vyovyote vinavyo hatarisha afya, usalama na maendeleo yao, kama vile
kujihusisha kwenye masuala ya ngono, matumizi ya madawa ya kulevya na vileo
katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo ya mitihani
yao. Watoto wetu wa Kike na Kiume wajitambue, na wajue kuwa wao ni hazina
ya pekee katika maendeleo ya nchi yetu. Kipindi hiki wakitumie vizuri kwa kuwa
waadilifu, waaminifu, wenye bidii na kuzingatia kanuni za nidhamu na tabia
njema huku wakijiandaa kwa ajili ya kuendelea na elimu ya Sekondari. Tukumbuke
kuwa Serikali imekusudia kumpa kila mtoto nafasi ya kupata elimu ya Sekondari.
Msingi tayari umeshawekwa na Rais wa Awamu ya tano, Mheshimiwa John Pombe
Magufuli wa kutoa Elimu ya Sekondari bure. Hivyo tusingefurahi mmojawapo kati ya
watoto hawa waliomaliza elimu ya msingi jana akaikosa nafasi hii kwa sababu
zinazoweza kuzuilika. Nawaasa watoto wote kutumia kipindi hiki kwa kukataa
kurubuniwa, kushawishiwa na kujiingiza katika mambo yenye kuhatarisha afya,
usalama na maendeleo yao.
Ninawataka Wazazi wenzangu, Walezi na
jamii kwa ujumla:-
(i)
Kutowaozesha watoto wote wa kike
waliohitimu darasa la saba mwaka huu wakati wa kipindi hiki cha kusubiria
matokeo yao, iwe ni kwa sababu yoyote ile au kwa lengo la kujipatia mali kwa
njia ya mahari. Kila Mzazi/Mlezi anapaswa kutambua umuhimu wa mtoto wake
kuendelea kielimu, na kukua kimwili na kiakili kabla ya kuingia katika ndoa.
Ieleweke kuwa Elimu ya watoto wa kike ni moja ya njia bora za kupunguza
umaskini katika mataifa yanayostawi. Kila mwaka wa elimu kwa mwanamke utaongeza mapato yake ya
baadae kwa asilimia 15, ikilinganishwa na asilimia 11 kwa wanaume. Aidha, Kila
mwaka wa mtoto wa kike kuwa shule humuepusha na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
(VVU) mara 7. Pia, uzoefu
unaonyesha kuwa, kila mwaka wa kuelimika humsaidia msichana kufanya maamuzi
bora yake na ya familia yake. Benki ya Dunia ilibainisha ya kwamba kila mwaka
wa elimu huzuia vifo 2 vya uzazi katika wanawake 1000 kila mwaka!. Kwa hiyo kumpa mtoto wa kike fursa ya elimu
inamsaidia sio yeye tu kukua kiakili na kimwili lakini pia inamnusuru na ndoa
na mimba za utotoni na kuchangia maendeleo yake, ya familia yake na jamii kwa
ujumla. Ni vyema jamii hasa wazazi na walezi wafahamu kuwa ndoa kwa
wasichana sio njia muafaka ya kutatua changamoto za kifedha za wazazi/walezi.
Bali elimu ndio njia bora ya kutatua changamoto hizo.
(ii) Kuwalinda watoto wote wa kike na wa
kiume waliohitimu darasa la saba mwaka huu dhidi ya vitendo vyote vya Ukatili, hasa
kwa watoto wa kike kupewa mimba au kuwahusisha katika mahusiano ya kimapenzi. Kwa
mujibu wa Sheria ya makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998 ambayo imefanyiwa
marekebisho na kuhuishwa kwenye Makosa ya Jinai (‘Penal Code Cap 16”) inaelekeza kuwa ni kosa la jinai kwa mtu yoyote kumlaghai mtoto wa chini ya
miaka 18 kwa kumpa mimba au kufanya nae
mapenzi. Kifungu cha 130 (e) cha Sheria hii
kinaeleza wazi kuwa “Ni kosa kwa mtu wa
jinsia ya kiume kumbaka msichana au mwanamke; kwa ridhaa au bila ya ridhaa akiwa
chini ya umri wa miaka kumi na nane”. Mtu yeyote atakayetenda kosa la
kubaka atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha au kifungo kisichopungua
miaka thelathini. Aidha, Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 Kifungu cha 83
kinaelekeza kuwa ni kosa kumuhusisha mtoto katika kazi, biashara au mahusiano yoyote
yenye mlengo wa kingono iwe ni kwa malipo au bila malipo.
Mkono wa Serikali ni mrefu.
Tutahakikisha tunawakamata na kuwafikisha Mahakamani wale wote watakao kwenda
kinyume na sheria hizi.
Aidha, natoa Rai kwa wananchi wote
kuendelea kutoa taarifa kwa mamlaka husika za Serikali za Mtaa, Kijiji, Kata,
Wilaya na hata katika Madawati ya Jinsia na Watoto yaliyopo Polisi, pale watakapobaini
mzazi au mlezi au taasisi anaenda kinyume na jitihada za serikali za
kumuendeleza mtoto kielimu hasa katika kudhibiti ndoa za watoto waliomaliza
Elimu ya Msingi hususan katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo yao.
“Vunja ukimya
toa taarifa kwa maendeleo ya watoto wetu”.
Nawatakia kila la kheri watoto wote wa
Tanzania katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo yao ya mtihani wa Elimu ya
msingi.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu wabariki watoto wa
Tanzania.
Imetolewa
na
UMMY
A. MWALIMU (MB)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE
NA WATOTO
DODOMA
09/09/2016
0 comments:
Post a Comment