na Erasto T. Ching’oro, Msemaji - Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto
Wadau wa Asasi za
Kiraia (AZAKi) walishiriki Tamasha la kumi na tatu lilioanza tarehe 1- 2
Desemba 2015 katika ukumbi wa Blue Pearl jijini Dar es salaam na kufunguliwa na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia an Watoto Bibi Sihaba
Nkinga.
Mgeni rasimi Bibi
Sihaba Nkinga, ametoa shukrani kwa shirika la the Foundation for Civil Society
kwa kuandaa Tamasha hilo lenye Kauli Mbiu: ‘Wajibu wa Asasi za Kiraia katika Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo
Endelevu 2030’.
Ameeleza
kufurahishwa na ari ya wadau wa AZAKi katika kuendelea kushiriki na kuchangia jitihada
za kuleta maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Ameongeza kuwa kauli mbiu ya Tamasha
la mwaka 2015 ni ushahidi tosha kuwa AZAKi na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni
wabia muhimu katika maendeleo
.
Akimkaribisha mgeni rasimi, Bibi DKT. Stigmata Tenga
ambaye ni Rais wa Foundation for Civil Society alibainisha malengo ya Tamasha kuwa
ni kutoa fursa kwa washiriki kujadili
na kuainisha masuala yatakayozingatiwa na jinsi ya kuimarishsa ushiriki wa
wananchi na Asasi za Kiraia (AZAKi) na kuyapa kipaumbele wakati wa utekelezaji
wa Malengo ya Maendeleo Endelevu. Aidha, Tamasha hilo litajenga
jukwaa kwa wadau wa AZAKi kujadili namna
ambavyo Foundation for Civil Society itaboresha huduma za kujenga uwezo wa
Asasi za Kiraia nchini kwa kutoa katika kuimarisha uwezo na huduma za asasi
kiutendaji na kiutawala.
Tamasha la Azaki linakutanisha takribani wadau
300 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini. Bibi Nkinga amaeleza kuwa fursa hii itatumiwa
na wadau kujenga uelewa wa pamoja kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu na
kuweka mikakati ya kukuza ushiriki katika utekelezaji wa malengo hayo kwa
kuzingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa jamii. Amewataka wadau kushiriki
katika kuandaa Malengo Mapya ya Maendeleo endelevu ya mwaka 2030 kusaidia
kuwafahamisha wananchi mchakato uliotumika kuandaa Malengo hayo na utekelezaji
wake ili kuondoa umasikini kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine.
Akifafanua Bibi Sihaba amewataka wadau kutumia Tamasha
la Azaki kujadili mafanikio na changamoto zilizopo katika utekelezaji wa Malengo
ya Milenia. Kwani majadaliano yao yataweka kuwa na uelewa wa pamoja na kuibua mipango
thabiti ya utekelezaji.
Itakumbukwa
kwamba, baada ya kutolewa kwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia yaliyopita, nchi
iliandaa mikakati ya kuitekeleza. Mikakati hiyo ni pamoja na MKUKUTA (Tanzania
Bara), MKUZA kwa Zanzibar na Mpango wa Maendeleo wa Miaka 5. Mikakati hii
ilikuwa na vipaumbele pamoja na viashiria vya kupima mafanikio na ufuataliaji
ili kufikia Malengo yaliyowekwa.
Katika
utekelezaji wa Malengo ya Milenia kama nchi tuliweza kupata mafanikio makubwa
katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na:
kuongezeka
kwa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa
mashuleni; kuongezeka kwa Idadi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi kama Bunge hadi kufikia Asilimia 30; ongezeko
la uwiano wa wanafunzi wa kike na wakiume katika shule za Msingi na shule za
Sekondari; kupunguza kwa Asilimia 70
(2/3) vifo vya watoto wenye umri chini
ya miaka 5; na kupungua kwa vifo vya mama na mtoto. Mengine ni kupungua kwa
kiwango cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa watu wenye umri kati ya miaka
15-24 na 25-49; na kuongezeka kwa idadi ya wananchi wanaotumia maji safi na
salama ya kunywa. Katibu mkuu Bibi Nkinga amaeleza kuwa mafanikio haya yamefikiwa
kwa ushirikiano thabiti wa AZAKi na Serikali.
Awali,
Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil Society Bw. Francis Kiwanga alieleza
kuwa Tamasha la AZAKi 2015 litakuwa na mada
nne ambazo ni: wajibu na
mikakati ya kuimarisha ushiriki wa asasi za kiraia katika utekelezaji wa Malengo
ya Maendeleo Endelevu; wajibu wa sektab binafsi katika utekelezaji wa Malengo
ya Maendeleo Endelevu; wajibu wa Serikali katika utekelezaji wa Malengo ya
Maendeleo Endelevu; na utunishaji mfuko na ugharamiaji wa Mpango wa Maendeleo
endelevu. Rai imetolewa kuzingatia upatikanaji wa rasilimali kutoka ndani na nje ya nchi katika kutekeleza Malengo
Endelevu ya Maendeleo.
Katibu Mkuu Nkinga amebainisha
kuwa, yeye anaamini kuwa bila Asasi za Kiraia makini zenye uzalendo zinazotanguliza
maslahi ya taifa hatutaweza kuwa na Tanzania tunayohitaka miaka ijayo. Hivyo
katika mijadala mnatakiwa kuzingatia wajibu mkubwa wa AZAKi kwa jamii katika
kuchangia kufikiwa kwa malengo ya maendeleo endelevu, tunapaswa kupitia upya
dhamira zetu na kuwa tayari kujifunza kwa wengine ili kuimarisha utendaji wa Asasi
zetu na kutoa mchango unaokusudiwa. Washiriki wamekumbushwa kufanyakazi kazi
kwa juhudi na maarifa ili kuunga mkono dhamira ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe
Magufuli ya kuwawezesha Watanzania kujiletea maendeleo yao na kuondokana na
umasikini kupitia kauli mbiu ya HAPA KAZI TU!
Watendaji
wa AZAKI wametakiwa kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa wadau mbalimbali hususan kwa
jamii, serikali, wanachama na wafadhili. Utamaduni huu ukiendelezwa sio tu
kwamba wadau wa Asasi za Kiraia watajijengea uhalali kwa wananchi na jamii bali
pia wataweza kuimarisha ubia na Serikal.
Mwisho, Katibu Mkuu Bibi
Nkinga aliwataka wadau wa Asasi za Kiraia kurejea maneno ya Muasisi
wa Taifa Letu Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutoka katika Kitabu
chake cha ‘Uhuru na Maendeleo’ ambaye aliwahi kusema: "Mtu
anaendelea ikiwa uwezo wake umekua au kipato chake kimeongezeka kumwezesha yeye
na familia yake kuishi maisha bora zaidi; Mtu haendelei kwa kutegemea kupewa
vitu na watu wengine” (1973).
0 comments:
Post a Comment