Kutokana na jitihada
za Serikali za kuweka mazingira wezeshi kupitia uratibu na uwezeshaji wa
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, mashirika haya yameendelea kutambuliwa na wadau
katika ngazi mbalimbali. Mipango mbalimbali ya kitaifa kama vile Mkakati wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania - II (MKUKUTA - II) na Mpango wa
Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/16) inayatambua mashirika haya kuwa
wadau muhimu katika uandaaji na utekelezaji wake. Aidha, Sera zote za kisekta
hapa nchini zinayatambua Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwa wadau muhimu
katika uandaaji na utekelezaji wa Sera husika. Katika kipindi cha Serikali ya
Awamu ya Nne, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yamekuwa washiriki muhimu katika
uandaaji na utekelezaji wa sera mbalimbali zikiwemo: Sera ya Afya (2007), Sera
ya Elimu na Mafunzo (1996), Sera ya Maji (2000), Sera ya Mazingira (2000), Sera
ya Maendeleo ya Jamii (1996), Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000)
and Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008).
Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne Wizara, Idara na
Wakala mbalimbali za Serikali na Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na
Majiji zimeendelea kuwa na ubia na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika
utekelezaji wa Sera mbalimbali za kisekta na Kitaifa. Ubia huo ulijikita katika
maeneo ya kukuza uelewa na ushiriki wa jamii katika maendeleo, ufuatiliaji na
tathmini ya utekelezaji wa miradi ya Serikali, utoaji wa huduma kwa jamii, uandaaji
na mapitio ya mipango na Sera mbalimbali.
Juhudi za Serikali
zimesaidia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoa mchango katika nyanja
mbalimbali za maendeleo. Kwa mujibu wa Taarifa ya Mchango wa Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali ya mwaka 2012, mashirika haya yaliwekeza kiasi cha shilingi 524.5
bln katika maeneo ya elimu, afya na Virusi Vya UKIMWI/UKIMWI, maendeleo ya
jinsia na utawala bora, mazingira, kinga ya jamii, maji na kilimo.
Wizara kupitia
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yametoa mchango katika kutengeneza nafasi za
ajira na fursa ya kujitolea kwa Watanzania. Taarifa ya Mchango wa Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya mwaka 2012 inaonesha kuwa Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali yaliajiri watu 33,388 na watu 27,312 walifanyakazi kwa
kujitolea. Kati ya hao, watanzania walioajiriwa walikuwa 32, 279 na watanzania
22,996 walipata fursa ya kujitolea katika mashirika mbalimbali.
Katika Sekta ya Afya
mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ulikuwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo matibabu kwa
wanawake wenye matatizo mbalimbali hususan fistula. Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali kupitia programu ya utengamao
inatolewa na Shirika Lisilo la Kiserikali la CCBRT limeongeza uelewa kwa jamii
kuhusu matibabu ya fistula kwa akinamama kuwa fistula inatibika hospitalini. Uelewa
huu umewezesha wakinamama wenye matatizo ya fistula itokanayo na uzazi kwenda
hospitali na kupata matibabu. Hospitali zinazotoa huduma ya Fistuli ni pamoja
na hospitali ya Seliani (Arusha), KCMC (Kilimanjaro), Kabanga (Kigoma) na
CCBRT, Dar es Salaam. Katika kipindi cha
2013 hadi 2014, jumla ya wanawake 868 wamepatiwa matibabu ya fistula itokanayo
na uzazi. Aidha, Programu ya utengamao inajumuisha kituo maalumu cha kuwapatia
ujuzi wanawake waliotibiwa fistula itokanayo na uzazi. Kituo hiki kinaitwa
“Mabinti” kiko jijini Dar es Salaam. Ujuzi unaotolewa na kituo ni pamoja na
ufundi cherahani; ufumaji; utengenezaji wa urembo na mapambo kwa kutumia
shanga; na utengenezaji wa mikoba
mbalimbali kutokana na mabango ya plastiki. Programu hii imewawezesha wanawake
waliokuwa na matatizo ya fistula kuweza kujumuika katika jamii
iliyokuwaimewatenga na hatimaye kujitegemea kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment