Serikali
inayatambua Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kuwa ni wadau muhimu katika
kupanua uhuru wa kujumuika na kuchangia katika maendeleo ya jamii na
taifa. Katika kipindi cha awamu ya nne,
Serikali iliendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya ushiriki wa Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali katika maendeleo na kukuza demokrasia na madaraka kwa
umma. Juhudi hizi za Serikali zilifanyika kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya
Mashirika Yasiyo Kiserikali na Sheria ya Mashirika Yasiyo Kiserikali Na.24 ya
mwaka 2002 iliyorekebishwa mwaka 2005. Katika eneo hili la utekelezaji, Serikali ilijikita katika usajili, uwezeshaji
na uratibu wa Mashirika Yasiyo Kiserikali.
Usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
Serikali iliendelea
kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kupanua uhuru wa wananchi kujumuika
kupitia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuyatambua kupitia usajili chini ya
Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
Na.24 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa mwaka 2005. Mwaka 2005
Serikali ilianza kutoa huduma za usajili chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo
Kiserikali Na.24 ya mwaka 2002 iliyorekebishwa mwaka 2005 ambapo hadi kufikia
Juni, 2014 jumla ya mashirika 6,679 yalikuwa
yamepatiwa usajili. Kati ya hayo, mashirika 5,835 yalipatiwa Cheti cha
Usajili na mashirika 844 Cheti cha Ukubalifu.
Katika kusogeza
huduma za usajili karibu na wananchi, mwaka 2010 Wizara iliwateua Maafisa
Maendeleo ya Jamii wa ngazi ya Mkoa, Halmashauri za Miji, Wilaya, Manispaa na
Majiji kuwa Wasajili Wasaidizi wa Wilaya na Mikoa husika. Aidha, Wizara ilitoa
mafunzo kuhusu uratibu na usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa maafisa
hao kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara ili kuboresha huduma za usajili na
uratibu. Mafunzo hayo yameongezea uelewa wa maafisa husika hivyo kuwajengea
uwezo wa kuwezesha hatua za awali za usajili.
Uratibu na Uwezeshaji wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
Kwa kutambua mchango
wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika maendeleo na ustawi wa jamii na taifa
kwa ujumla, Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali za kuongeza ushiriki na
kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika haya ili kutoa mchango mkubwa katika
kuondoa umasikini katika jamii. Hatua hizo ni pamoja na: kuhamasisha ubia baina
ya Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali; kuimarisha mawasiliano na
upatikanaji wa taarifa za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali; kutoa elimu ya Sera
ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001 na Sheria ya Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali Na.24 ya mwaka 2002; kuimarisha uwazi, uwajibikaji na
mifumo ya kujitawala miongoni mwa NGOs; na kutambua mchango wa Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali katika jamii.
Katika kukuza
uwajibikaji na fursa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kujitawala, mwaka 2008
Serikali ililiwezesha Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuandaa
Kanuni za Maadili ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Kanuni hizi zilitangazwa
kwenye Gazeti la Serikali (Taarifa ya Kawaida Na.363) la tarehe 5 Desemba,
2008. Kanuni hizi pia zilitafsiriwa katika lugha ya Kiswahili ili kurahisisha
matumizi yake kwa ajili ya kuyawezesha mashirika hayo kujitawala. Jumla ya
nakala 6,500 za Kanuni hizi zilisambazwa kwa wadau kutoka katika Serikalini na
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kipindi mwaka 2009 hadi 2014.
Wizara imeendelea kuboresha mazingira kwa ajili ya kukuza
ubia na uwazi katika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Hii ni pamoja na
kuhamasisha ubia katika maendeleo na uandaaji wa Sera za Kitaifa na kisekta
miongoni mwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.
Mikutano baina ya Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wadau
imeendelea kufanyika katika ngazi ya mikoa ikitumika kuhamasisha ubia katika
ngazi mbalimbali za utendaji.
Serikali kupitia
Wizara YA Maendeleo Ya Jamii Jinsia na Watoto imeendelea kuwezesha upatikanaji
na ubadilishanaji wa taarifa za NGOs kwa wadau. Hii ni pamoja na kuanzisha na
kuendesha Tovuti ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (http//www.tnnc.go.tz)
na Benki ya Taarifa na Takwimu za Uratibu wa NGOs ambapo jumla ya wadau 30,679
walinufaika na huduma hii katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi kufikia
mwaka 2014. Taarifa hizo ziliwawezesha wadau kutoka Serikalini, Taasisi za
Elimu ya Juu na Utafiti, Taasisi za Fedha hususan mabenki na Wabia wa
Maendeleo kufanya maamuzi sahihi katika
masuala yanahusiana na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Bibi Gizere Hamisi Mwenye Umri wa Miaka 78 Kutoka
katika Kijiji cha Ngasemi Kata ya Ubetukahe, Wilaya ya Rombo akiwa na Mtoa
Huduma za Kisheria Kutoka Shirika Lisilo la Kiserikali (AJISO). Kutokana na
huduma hii Bibi Gizere Ambaye ana Watoto
wa Kike tu Amewezeshwa Kumiliki eneo la Ardhi hii baada ya Kuachana na Mume
wake.
|
Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne,
Wizara kupitia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ikiwemo AJISO yametoa elimu
kuhusu Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 na kutoa huduma za kisheria kwa wanawake
ambao waliipoteza kutokana na vikwazo vya kimila. Aidha, Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali yamewawezesha wasichana waliokuwa wakifanyakazi zisizo za kistaha
hususan wafanyakazi wa majumbani kupata elimu ya fani mbalimbali na kuwapatia
vifaa vya kuwawezesha kujiajiri na kuajiri wenzao. Vilevile, AJISO na wadau wengine wametoa
msaada wa kisheria kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Mchango wa Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali yanayoratibiwa na Wizara ikiwemo CCBRT yamewezesha watoto wenye mahitaji maalum
wakiwemo wenye ulemavu wa viungo kuandikishwa katika shule na kupata elimu.
CCBRT pia imetoa mafunzo kwa walimu na wazazi kuhusu haki za watoto kupata
elimu. Pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu na wazazi pia huwapatia watoto wenye
ulemavu wa viungo viti maalumu na madawati maalumu kulingana na ulemavu walio
nao. CCBRT imeendelea kutoa elimu kwa walimu na wazazi kuhusu miundombinu
rafiki ikiwa ni pamoja na vyoo, madarasa na mazingira ya shule kwa ujumla.
CCBRT imewafundisha wanafunzi kuhusu ulemavu na namna ya kuwasaidia wenzao
wenye ulemavu wakiwa shuleni na nyumbani. CCBRT imewalipia ada ya shule na
usafiri watoto wenye ulemavu ambao wazazi wao hawana uwezo. Katika kipindi cha
2005 hadi kufikia 2014 jumla ya watoto 477 wenye ulemavu mbalimbali walikuwa
shule za msingi jijini Dar es Salaam kuanzia 2005 mpaka 2014. Kati yao watoto
173 mpaka 2014 waliweza kumaliza Elimu ya Msingi na watoto 17 walichaguliwa
kuendelea na Elimu ya Sekondari. Vilevile, CCBRT imetoa huduma ya utengamao kwa
wanawake wenye fistula na watoto wenye ulemavu.
0 comments:
Post a Comment